Kwa heri, TESA wa HUBA
Tasnia ya burudani nchini imepata pigo kubwa kufuatia kifo cha mwigizaji maarafu, Grace Mapunda, al maarufu Tesa ambae alikua akicheza katika tamthilia maarufu ya Huba. Mama yetu Grace Mapunda umauti ulimkuta tarehe 2 Novemba 2024 katika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Kikazi, Grace amekuwa katika tasnia ya burudani kwa zaidi ya miaka 20. Mashabiki walimpenda kwa ucheshi wake na uigizaji wake wa kipekee.
Alikuwa kiungo muhimu sana katika familia ya Huba. Kifo chake kimeacha pengo katika mioyo ya watu, wakiwemo waigizaji wenzake.
Hili linadhihirika kwa kuona jinsi viongozi wa dini na serikali, wasanii wenzake na waombolezaji mbalimbali walijitokeza viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam, Tarehe 4 Novemba2024 kwa ajili ya kumuaga marehemu Grace Mapunda na baadaye kuzikwa katika makaburi ya kinondoni.
Rais Dkt Samia Suluhu Hassan alijiunga kuomboleza msiba na Watanzania kupitia ukurasa wake rasmi wa Instagram akisema “Ninatoa salamu za pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na wasanii hasa waigizaji wa filamu nchini kwa kuondokewa na ndugu yetu, Grace Mapunda. Kwa Zaidi ya miaka 20 Grace ametumia kipaji chake kutupa burudani na kuelimisha mamilioni ya watanzania kupitia tsanaa yake ya uwigizaji. Mwenyezi Mungu ampumzishe pema Peponi.
Kwa Heri, TESA wa HUBA